Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Kufuatia kisa ambacho vijana waliwavamia wakazi ambao walikuwa wakiadhimisha siku ya Eid kwenye uga wa umma wa Makadara wiki jana, Idara ya polisi imetakiwa kuweka usalama katika mji wa Mombasa wakati kunakuwa na sherehe kuu za kuadhimisha siku maalum za taifa na kidini.

Kulingana na wakazi kutoka mji wa kale jijini Mombasa, nyakati za siku kama hizi huwa na shughuli nyingi, na mara kwa mara kumekuwa na visa vingi vya ukosefu wa usalama miongoni mwa wakazi.

Wakiongozwa siku ya Ijumaa na mshirikishi na mwanaharakati wa masuala ya usalama wa mitaa Alfan Abdul, kitendo cha vijana kuingia kwenye uwanja huo wa umma na kuanza kuwapiga watu na kupora mali, ambapo watu watatu walijeruhiwa vibaya kwenye makabiliao hayo.

Abdul aliwataka maafisa wa polisi kuwajibikia kazi yao ya usalama, na kudai kuwa vijana ambao walihusika kwenye uhalifu huo wangezuia kutenda uhalifu huo na kusema si vizuri maafisa kujitokeza wakiwa wamechelewa na baada ya watu kupigwa na kujeruhiwa.

Kwa sauti moja wakazi hao walitoa wito kwa serikali kuu na hasa serikali ya kaunti ya Mombasa kutafuta njia ya kuwapa vijana kazi ili kujiepusha na uhalifu mitaani, na kumtaka gavana wa kaunti hiyo kuajiri kikosi maalum cha askari kupiga doria kwa ushirikiano na maafisa wa polisi ili kuboresha usalama ambao unaendelea kudorora kwenye jiji hilo la utalii.