Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Kufuatia madai ya familia moja kutoka kaunti ya Mombasa kuwa polisi ndio waliohusika katika kumteka nyara mwanao ambaye hajulikani aliko, kamanda wa polisi wa kanda ya pwani Francis Wanjohi amejitokeza kukana madai hayo.

Wanjohi ametetea maafisa wa polisi na kusema kuwa huenda mtoto huyo alitekwa na magenge ya wahalufu ambao wamechukua nafasi ya ukosefu wa usalama.

"Polisi wanatafuta mtu ambaye ana jina sawa na hilo lakini hatuna uhakikika kuwa ndiye huyo na uchunguzi umeanzishwa na idara ya polisi, na si polisi walihusika kumshika anayesemwa," alisema Wanjohi.

Kamishna huyo aliwataka wakazi kuwa macho wanapotembea hasa nyakati za usiku, ambapo imekuwa mara kwa mara usalama wa wakazi humo hatarini.

Wanjohi alikuwa akiongea na wanahabari siku ya Jumanne baada ya familia ya kijana Samir Said, ambaye inadaiwa alitekwa nyara na watu ambao jamaa yake imedokeza kuwa walikuwa maafisa wa polisi.

Kulingana na mmoja wa jamaa wa kijana huyo, Said Munir ambaye ni mjomba, kijana wao hana hatia yoyote na anawashtumu polisi kwa kuhusika kwa kupotea kwa mwanao, ambaye alikuwa msanii.

Kwa siku za hizi karibuni, wakazi wengi kutoka eneo zima la pwani wamekuwa wakiwalaumu maafisa wa usalama kwa kuchangia kupotea jamaa zao, madai ambayo idara ya polisi imekanusha.