Wanaoweka muziki kwa sauti ya juu katika mji wa Kisii wameonywa na kuombwa kupunguza sauti ya muziki au kuchukuliwa hatua za kisheria.
Akiongea siku ya Alhamisi ofisini mwake ilioko mjini Kisii, Afisa mkuu wa NEMA katika Kaunti ya Kisii Samson Bokea aliwaomba watu hoa haswa waonaofanya biashara katika klabu karibu na hospitali ya Rufaa na Mafunzo ya Kisii na shule katika mji wa Kisii kupunguza sauti za muziki wao.
Aidha, Bokea alisema kuwa kufuatia malalamishi kutoka kwa wananchi wanaoishi karibu na duka hizo, wameamua kuchukua hatua hiyo kama idara husika ili kuleta suluhu mwafaka.
"Kutokana na malalamishi nimeyapata kutoka kwa wananchi wengi ambao wanakuja ofisini mwetu, naomba wafanyibiashara hao kupunguza muziki wao kwani si kila mtu ananufaika na muziki huo," alihoji Bokea.
Kwa mujibu wa Bokea, kuna klabu kimoja karibu na Hospitali ya Kisii ambacho kimewasumbua wagonjwa kwa makeleke wa muziki wanaoweka usiku.
Kwingineko, Afisa huyo alisema kuwa kelele hiyo si afya kwa watoto wadogo kwa sababu inadhuru afya ya mtoto anapokua, haswa wengi huwa na shida ya kushtuka.
Kwa sasa amewaomba wamiliki wote wa vilabu kuchukulia swala hilo kwa uzito ili kuboresha viwango vya mazingira katika Kaunti ya Kisii.
Afisa Bokea ametoa onyo kali kwani mwenye kupuuza agizo hilo kuwa atachukuliwa hatua kali ya kisheria.