Share news tips with us here at Hivisasa

Seneta wa kaunti ya Nyamira Kennedy Mong’are Okong'o amewaomba machifu wote na manaibu wao katika kaunti ya Nyamira kushirikiana na maafisa wa polisi kupunguza visa vya uhalifu katika kaunti hiyo.

Wito huo umetolewa baada ya kubainika kuwa visa vya uhalifu ambavyo hutekelezwa na washukiwa wa ujambazi vimekuwa vikiongezeka katika siku za hivi maajuzi katika kaunti hiyo, jambo ambalo limemlazimu Seneta Okong'o kushauri machifu kushirikiana na polisi ili kupunguza visa hivyo.

Usiku wa kuamkia siku ya Jumapili washukiwa wa ujambazi walibomoa nyumba ya mtu na kumshambulia katika eneo la Sironga kaunti ya Nyamira. Kwa bahati nzuri akaokolewa na watu baada ya kupiga nduru huku majambazi hao wakifanikiwa kutoroka.

Akizungumza mnamo siku ya Jumapili katika eneo la Bogichora, eneo bunge la Mugirango Magharibi ambapo visa vya uhalifu vimekuwa vikiongezeka, Seneta Okong'o alisema machifu na manaibu wao wakishirikiana na polisi, visa vya uhalifu vitapungua katika kaunti ya Nyamira kwa kiasi kikubwa.

“Naomba machifu na manaibu wao katika kaunti nzima ya Nyamira  kushirikiana na polisi ili visa vya ujambazi na uhalifu mwingine uweze kupunguzwa katika kaunti yetu ya Nyamira,” alisema Okong’o.

Aidha, Seneta huyo  aliomba mkuu wa polisi katika kaunti ya Nyamira kuagiza maafisa wa polisi kuimarisha usalama nyakati za usiku ili kupambana na washukiwa wa ujambazi  ambao huangaisha wakazi wa kaunti hiyo.