Afisa mkuu anayesimamia mikasa katika serikali ya kaunti ya kisii amesema serikali ya kaunti hiyo itagharamia shughuli zote za mazishi ya kijana aliyeaga dunia katika eneo la Nyambera.
Hii ni baada ya kijana mmoja kupoteza maisha yake alipokuwa akikwangura kokoto na kuangukiwa na mawe katika eneo hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano katika eneo hilo la Nyambera, baada ya mkasa huo, Patrick Lumumba alisema serikali ya kaunti itahusika vyovyote vile katika familia ile iliyopoteza mwenzao kwa hali ya kutatanisha kuhakikisha mazishi yamekamilika vilivyo.
Afisa huyo alisema kikosi cha kushughulikia mikasa kitafika katika eneo hilo siku ya Alhamisi ili kuangalia jinsi eneo hilo lilivyo ili kutoa ilani ya kuruhusu au kukataza vijana hao wa kukwangura kokoto kufanya kazi katika eneo hilo.
Alisema kuwa maisha ya watu wengi yako wanaofanya kazi katika timbo hilo yakohatarini.
Mwenyekiti wa vijana ambao wanakwangura kokoto katika eneo hilo Gilbert Ongwae alisema kuwa kijana ambaye alipoteza maisha yake ni wa tatu kupoteza maisha katika eneo hilo kwa muda miaka ishirini na mitano iliyopita.
“Tunahofia kuwa maisha ya vijana hawa ambao wanakwangura kokoto katika eneo hili yako hatarini. Tutahakikisha kuwa kikosi cha mikasa kitakuja hadi eneo hili ili tuweze kujadili ikiwa vijana ambao wanafanya hii kazi wataendelea na kazi yao ama watalazimika kutafuta kazi zingine," alisema Lumumba.