Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Serikali ya Kaunti ya Kisii imeombwa kujenga vyoo katika soko la Kegogi iliyoko eneo bunge la Kitutu Chache Kaskazini ili kuinua hali ya usafi na kutunza mazingira mema.

Ombi hilo limetolewa na wafanyibiashara wa soko hilo ambao walisema kuwa hawana mahala pa kujisaidia wanapoendelea na shughuli zao za biashara katika soko hilo hasa siku za soko.

Wakiongea na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatano katika soko hilo, wafanyibiashara hao wakiongozwa na Mary Ondima waliomba serikali ya Kaunti ya Kisii kuwajengea vyoo kwani wamekuwa wakisumbuka kwa muda mrefu hasa wanapohitaji kuenda haja ndogo.

Kulingana na wafanyibiashara hao, soko la Kegogi ni moja ya masoko makubwa katika kaunti ya Kisii kwa ubadilishanaji baina ya Jamii tatu za Kisii, Luo na Maasai pamoja na kujumuisha wafanyibiashara wengine kutoka kaunti zingine.

“Sisi wafanyibiashara tumekuwa tukisumbuka sana hasa siku za soko kwa kuwa hatuna mahali pakujisaidia. Vyoo ambavyo vilikua hapa vimeisha na huwezi enda huko kama unahitaji kujisaidia,” alisema Samwel Keng’oina, mfanyibiashara.

“katika serikali ya kaunti yetu, mengi yamefanyika lakini gavana wetu anapaswa kujua kuwa usafi ni swala muhimu sana hasa mahali kama hapa ambapo tunauza chakula. Swala hili linapaswa kushughlikiwa haraka,” alisema Martha Bosire, mfanyibiashara.

Wafanyibiashara hao walisema kuwa ni swala la aibu kwa soko kama hilo kutokuwa na mahali pa kujisaidia ilhali huletea kaunti hiyo pesa kupitia ushuru inayotozwa.