Share news tips with us here at Hivisasa

Gavana wa Kaunti ya Kisii James Ongwae ameombwa kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo serikali yake ilianzisha katika wadi ya Moticho.

Wito huo umetolewea baada ya miradi ya maji, elimu na ukarabati wa barabara kuanzishwa katika wadi hiyo ya Moticho mwaka wa 2013-2014 na kukwama kukamilika.

Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatano ofisini mwake, mkuu wa wilaya ya Moticho, Kingsley Matagaro alisoma ripoti ya wakazi waliokuwa wakilalamikia kutomalizwa kwa miradi ya maendeleo katika wadi ya Moticho.

Wakazi hao walisema hakuna mradi ambao serikali ya kaunti ya Kisii imeanzisha na kukamilisha katika wadi hiyo.

Kulingana na ripoti yao iliyosomwa, barabara za kutoka Nyakeyo-Nyabera, Arura-Nyabiosi na ile ya Ruma-Getiongo zilianzwa kukarabatiwa mwaka wa 2013 na hadi sasa hazijakamilika.

Wakazi hao walisema kuwa ujenzi wa madarasa ya chekechea katika shule ya msingi ya Nyabiosi na Nyamesari ulianzishwa lakini bado haujakamilika.

“Tumefwatilia kwa nini miradi yetu inakwama lakini hadi sasa hakuna jibu tumepata na tunaomba Gavana Ongwae atukumbuke na akamilishe miradi hiyo maana sisi sote ni wa kaunti ya Kisii,” alisema Kingsley Matagaro.

Mwakilishi wa wadi hio ya Moticho, Evans Mokoro, aliikosoa serikali ya kaunti na kusema hajui kwa nini serikali inaanzisha miradi na kushindwa kuikamilisha.