Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kaunti ya Mombasa imekosolewa kwa kushindwa kurekebisha mabomba ya majitaka na mitaro hali ambayo huenda ikasababisha maradhi ya kiafya.

Kulingana na mkurugenzi mkuu wa Shirika la Kimazingira la ‘Eco-Ethics International and Environmental Conservation Organisation’, Daktari Bernard Okeyo, serikali ya kaunti hiyo imezembea katika majukumu yake ya kuimarisha maswala ya kimazingira.

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Okeyo alidai kwamba swala hilo limedumu kwa muda na wala hakuna hatua zozote serikali ya kaunti hiyo imechukua kurekebisha swala hilo ila kutegemea Shirika la Msalamba Mwekundu kuwasaidia kila mara.

“Viongozi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa wameshindwa kuwajibikia majukumu yao swala ambalo limechangia mazingira duni kwa wakazi. Hatujaona wakianza kurekebisha mabomba ya majitaka ili kusaidia kupitisha maji wakati wa mvua,” alisema Okeyo.

Okeyo alisema kuwa endapo kutashuhudiwa mvua ya El Nino, basi wakazi wengi watataabika kwasababu maeneo wanayoishi hayapo salama ikizingatiwa kuwa wakazi wengi wanaishi katika maeneo ya vitongoji duni.

Alisema kuwa maeneo ya Changamwe, Jomvu, Mishomoroni eneo la Kisauni na Mburukenge, Moroto eneo la Tudor yako katika hatari kubwa zaidi ya kuathirika na mafuriko iwapo serikali ya kaunti hiyo haitachukua hatua za dharura kurekebisha maeneo ya mabonde ili kuzuia maporomoko.

Kauli ya mkurugenzi huyo mkuu wa shirika hilo la kimazingira imejiri baada ya idara ya utabiri wa hali ya anga kusema kuwa huenda kukashuhudiwa mvua ya El Nino kuanzia mwezi wa Octoba.