Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Madereva wa kituo cha magari kilichoko mji wa Kisii wamepongeza serikali ya kaunti ya Kisii kwa kuanza ukarabati wa kituo kipya cha magari.

Hii ni baada ya kituo hicho cha magari  kuharibika na kutatiza shughuli za uchukuzi haswa mvua inaponyesha kwani maji yalikuwa yanaterema katika kituo hicho.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika kituo hicho kilichoko katika mji wa Kisii, madereva hao wakiongozwa na Walter Obare walimpongeza Gavana wa kaunti ya Kisii James Ongwae kwa kuanza ukarabati wa kituo hicho na kusema ni njia moja ya kuinua na kuimarisha sekta ya uchukuzi katika mji wa Kisii.

“Tunapongeza serikali yetu ya kaunti kwa kuanza ukarabati wa kituo hiki ambacho kimekuwa kikitusumbua kwa muda mrefu sasa. Tunaomba serikali iendelee kufanya hivyo kwa vituo vyote vya magari katika kaunti hii ya Kisii,”alisema Sospeter Momanyi, dereva.

Wakati huo huo, madereva hao waliomba seikali ya kaunti ya Kisii kuwawekea mabango ya kuonyesha magari fulani yanaenda upande fulani ili abiria wasiojua mahali pa kupandia gari haswa wale wageni waweze kusoma mabango hayo na kujua pa kuenda.

“Tunaomba serikali iendelee kuleta maendeleo kama haya kwa kutengeneza steji zote ili sekta ya uchukuzi iweze kuimarika  zaidi,” alisema Solomon Kerama, dereva.