Mwenyekiti wa kikundi cha ‘Maono Youth group’ Daniel Omweri ameiomba serikali kuongeza kiwango cha pesa katika hazina ya Uwezo Fund na 'Youth Enterprise Fund' ili kuinua na kuimarisha maisha ya vijana nchini.
Wito huo umetolea baada ya kuonekana kuwa kupitia pesa hizo, idadi kubwa ya vijana imeweza kujiimarisha kupitia miradi mbalimbali hasa ufugaji wa kuku, nyuki na samaki.
Akiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano katika wadi ya Sensi, Omweri alisema pesa hizo za mikopo zimewasaidia vijana wengi hasa wale tayari wamekuwa wamepoteza tumaini katika maisha yao na kuomba kuongezewa pesa zaidi ili kufukuza hali ya umaskini katika Jamii.
Mwenyekiti huyo aliwaomba vijana wale ambao hawajajiunga na kikundi chochote wafanye hivyo ili kunufaika na mradi wa pesa hizo za serikali.
“Naomba wabunge wote wa bunge la kitaifa kujaribu kila wawezalo ili kushinikiza serikali kuongeza fedha zaidi kwa hazina ya Uwezo ili idadi kubwa ya vijana kunufaika na mradi huo,” alisema Omweri.
Kulingana na mwenyekiti huyo, vijana hawastahili kutumiwa na wanasiasa ila wanapaswa kutafuta lolote ambalo litawasaidi kujiendeleza kimaisha.
Alisema kikundi chake kimeimarisha maisha ya wanachama wake baada ya kuanzisha miradi mbalimbali inayowapa ajira dhabiti hasa kupitia ufugaji wa kuku.
“Natumai ifikapo mwezi wa 12 mwaka huu katika kikundi chetu tutakuwa tumekadiria faida ya zaidi ya Sh400,000 ambayo itatokana na mauzo ya kuku, mayai na nyama,” aliongezea Omweri.