Mwenyekiti wa watoto ambao hawana uwezo wa kuelewa na kuongea katika shule ya msingi ya Kisii, Pamela Bosire ameomba serikali kutoa pesa za watoto hao ili ziweze kuwasaidia kuendelea na masomo yao kama hapo mbeleni.
Akiongea na waandishi wa habari siku ya Jumatatu katika shule hiyo iliyoko mjini Kisii, mwenyekiti huyo ambaye pia ni mwalimu wa watotot hao aliomba serikali kutoa pesa za watoto hao hadi shuleni humo kwani wamekuwa wakisumbuka sana kwa ukosefu wa pesa ili watoto hao kuendelea na masomo na hata kupata chakula.
“Kazi ya kuwalinda watoto hawa ni ngumu sana maana hata pesa hatuna na wanafunzi hawa wanaendelea kuongezeka kila wakati. Serikali haitusaidii na pesa ambazo zinaweza kuwezesha wanafunzi hawa kulindwa kwa njia nzuri na kuendelea na masomo yao," alisema Bosire.
“Serikali yetu hapo mbeleni ilikuwa inatusaidia kwa kutukabidhi pesa hizo lakini ikafika mahala serikali ikakoma kutukabidhi pesa hizo. Ombi letu kwa serikali ni kutukabidhi hizo pesa ili kuinua elimu kwa watoto hawa,” aliongezea Bosire.
Wakati huo huo, mwenyekiti huyo aliomba serikali kuwanunulia wanafunzi hao vifaa ambavyo vitawasaidia wanafunzi hao kufanyia mazoezi na hata vile vifaa vingine ambavyo vitawawezesha kujifunza kufanya kazi ya mikono ili waje kujisaidia nyakati zijazo kupitia kufanyia kazi ya mikono.
Mkurugenzi huyo alisema huwa changamoto zingine zinazowakumba wanafunzi hao ni gareji ya magari ambayo imewekwa karibu na shule hiyo ambayo huwaathiri masikio yao kwani hawataki kelele kamwe na kuomba serikali kutafuta suluhu kuhusiana na shida hiyo.