Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Serikali ya kaunti ya Kisii imeombwa kuwaondoa watoto wanaorandaranda katika mji wa kisii.

Wito huo umetolewa baada ya wafanyibiashara wa mji huo kulalamika kuwa watoto hao wanawakosea heshima.

Wakizungumza na mwandishi huyu wa habari siku ya Jumatatu katika mji wa Kisii, baadhi ya wafanyibiashara walisema watoto hao wamekosa heshima baada ya mmoja wao kumvua mfanyibiashara mmoja nguo siku ya Jumapili jioni katika sehemu yao ya kuuzia mboga karibu na kituo cha magari ya kwelekea eneo la Keroka mjini Kisii.

“Chokoraa mmoja alikuja bila sisi kujua fikira zake na kumvua mmoja wetu nguo kisha akatoroka,” alisema Lydia Makori, mfanyibiashara.

Aliongezea: “Watoto hao wametusumbua sana katika mji huu wa Kisii. Tunaomba serikali ya kaunti kutafuta mbinu ya kuwafurusha hapa mjini Kisii au iwajengee shule iwachukue maana wametukosea heshima sisi kama wafanyibiashar.”

Beatrice Moraa, muuza mboga mjini Kisii, alisema watoto hao wamekuwa wakiongezeka kila mara na kuombaomba pesa katika mji huo wa Kisii huku wanaponyimwa, wanaanza kutusi wale ambao hawapeani pesa.

“Tumehofia maisha yetu maana tunapowanyima pesa wanatutishia. Pia wanasumbua wateja wetu wanapokuja kununua mboga zetu maana mteja anapoona hivyo, anaamua kuenda bila kununua chochote na hiyo ni hasara kwetu,” alisema Divinah Kerunda mfanyibiashara.

Serikali imeombwa kutafuta suluhu kwa haraka kwani baadhi ya watoto hao hutembea bila nguo, jambo ambalo limewakera na kuwashangaza wafanyibiashara.