Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Huku siku ya makazi ulimwenguni (World Habitat Day) ikisherehekewa siku ya Jumatatu , wakazi kutoka mtaa wa Dunga Unuse, eneo bunge la Jomvu, wameitaka serikali kuwafidia kwa kubomolewa majengo yao na kufurushwa kutoka kwenye makao yao.

Mkurugenzi mkuu wa shirika la kutetea haki za umma nchini Kenya, Amnesty International, alishangazwa na jinsi serikali imekuwa ikiwadhulumu wakazi na kuwabomolea makazi yao bila kuwapa fidia wala kuwapa njia mbadala ya kujikimu na kuendelea na maisha yao.

Akiongea kwenye hafla hiyo siku ya Jumatatu, katika eneo la Bangladesh, Justus Nyang’aya, alisistiza uwepo wa uwazi katika kuongoza umma na kuishauri serikali kuchukua nafasi nzuri na kuwashirikisha wakazi katika masuala muhimu yanayo wahusu.

“Serikali yoyote ile ni sharti iwajibikie umma. Kukitokea suala kama hili la watu kufurushwa kutoka mahali wanaishi, watu hawa wanahitaji kupewa fidia ya kuwafanya waendelee na maisha yao,” alisema Nyang’aya.

Alipendekeza kuwa wakazi wote ambao wameathiriwa kupewa ridhaa ambayo itawakimu kuendelea katika masuala ya biashara au ukulima ili uchumi wao upate kuimarika.

Baadhi ya wakazi ambao waliathiriwa kwenye ubomozi kwenye mtaa wa Dunga Unuse ambao waliongea na mwandishi habari huyu, walitoa hamaki zao kufutia kufurushwa makwao.

Walidai kuwa serikali kuu imekuwa na mtindo wa kuwaruhusu watu walio na pesa kuwadhulumu watu walio na kipato cha chini kwa kuwapokonya mali yao kwa nguvu.