Share news tips with us here at Hivisasa

Serikali ya Kenya imetia sahihi mkataba wa Sh34 bilioni na nchi ya Italia ili kufadhili mradi wa ujenzi wa bwawa la maji katika eneo la Kuresoi, Kaunti ya Nakuru.

Fedha hizo zitatolewa na benki mbili za Italia ambazo ni BNP Paribas na Lutesa San Paolo ili kugharamikia mradi huo. Hafla hiyo ambayo ilishuhudiwa na Rais Uhuru Kenyatta na Waziri Mkuu wa Italia Matteo Renzi ilifanyika katika ikulu ya rais jijini Nairobi baada ya wawili hao kufanya mazungumzo ya kuboresha uhusiano baina ya nchi hizo mbili.

Fedha hizo zitafadhili mradi huo kikamilifu ambao unajumuisha ujenzi wa bwawa la maji, mkondo wa maji na kitengo cha kutibu maji kilicho na uwezo wa kuingiza maji lita 100,000 kwa siku.

Mradi huo unatarajiwa kufaidi wananchi wa Kuresoi, Molo, Njoro, Rongai na mjini Nakuru. Akiongea kwenye hafla hiyo iliyohudhuriwa na Waziri wa biashara na maswala ya kigeni Amina Mohamed, Rais Kenyatta alikaribisha kampuni zaidi za Italia kuekekeza nchini kwani ugatuzi umetengeneza nafasi nyingi za uekezaji kwenye sekta kama vile kilimo, barabara, kawi na madini.

"Tupo makini kuhakikisha maendeleo yanatekelezwa kwenye kila sekta nchini kwa hiyo nachukua fursa hii kukaribisha kampuni zaidi za Italia kuekeza nchini," alisema Rais Kenyata.

Makubaliano hayo ya ufadhili yameongeza fedha zilizotolewa na nchi hiyo kwa kusaidia Kenya kufikia Sh59.3 bilioni.