Katibu wa chama cha Knut tawi la Masaba Kaskazini, Kaunti ya Kisii Meshack Obonyo ametoa onyo kali kwa shule za kibinafsi zinazoendelea kutoa mafunzo kwa wanafunzi.
Obonyo amezionya shule zile zinazoendelea kutoa mafunzo hayo na kuzipa makataa ya kuzifunga shule hizo kabla wanachama wa Knut na walimu wengine hawajafika hapo na kuzifunga.
Hii ni baada ya baadhi ya shule za kibinafsi katika Kaunti ya Kisii kuendelea kutoa mafunzo kinyume na walimu wa serikali ambao walisema wanahitaji shule za kibinafsi kuungana nao kulalamikia mshahara duni na kupokezwa nyongeza yao ya mshahara.
Akizungumza siku Jumanne katika mji wa Keroka wakati walimu hao walikuwa wakiandamana kulalamikia kutopokezwa nyongeza yao ya mshahara, Obonyo alisema wataelekea kwa shule za kibinafsi na kuzifunga mara moja.
Aidha, katibu Obonyo alisema shule za kibinafsi zinastahili kuungana nao ili kuendeleza mgomo hadi waongezewe mshahara wao.
“Kwa matawi 110 ya chama cha Knut, hakuna kurudi nyuma hadi tupewe nyongeza yetu ya mishahara. Walimu wa shule za kibinafsi wanapswa kufunga shule hizo na kutuunga katika mgomo huu,” alisema Obonyo.
Hii ni wiki ya pili tangu mgomo wa walimu uanzishwe nchini huku walimu wakiendelea kuapa kutorudi kazini iwapo hawataongezewa mshahara wao jinsi mahakama kuu ilivyoagiza.