Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Kitutu Masaba katika Kaunti ya Nyamira Timothy Bosire amemwomba Spika wa Bunge la Kaunti ya Nyamira Joash Nyamoko kutojihusisha kazi yake na siasa na kufanya kazi ipasavyo.

Akizungumza na Wandishi wa habari siku ya Alhamisi katika eneo la Mochenwa, Mbunge huyo alimtaka Spika Nyamoko kutoingilia masuala ya kisiasa haswa kumtetea Gavana wa kaunti hiyo John Nyagarama bungeni na kusema kazi hiyo ya kumtetea gavana inafanywa na kiongonzi wa walio wengi bungeni, wala sio spika huku akisema sharti aheshimu mamlaka hayo vile katiba inahitaji.

"Naomba spika wa bunge ya Nyamira kufuata sheria jinsi inasema. Mambo ya kujaribu kujiweka kwa masuala ya kisiasa sio halali na spika kufanya hivyo ni kuivunja sheria,” alisema Mbunge Bosire.

Haya yanajiri tu baada ya viongonzi tano kutoka Kaunti ya Nyamira kuandamana moja kwa moja hadi ofisi ya Gavana Nyagarama siku ya Jumatatu wiki hii wakitaka kujua jinsi serikali ya kaunti hiyo imetumia pesa za kaunti hiyo jambo lililozua rabsha.

Wakati uo huo, Wabunge hao tano walidai kuwa Gavana Nyagarama hajaweka wazi matumizi ya pesa za kaunti hiyo wakiongeza kuwa gavana huyo amekuwa akiajiri wafanyikazi kutoka ukoo wake madai ambayo yalikanushwa na Gavana Nyagarama.