Jumuia ya Waislamu nchini Kenya Supkem inaitaka serikali ya Saudia kuwajibikia maafa yaliyotokea wiki jana baada ya mkanyagano ambao ulisababisha vifo vya karibu mahujaji elfu moja na kuitaka serikali hiyo kuwafidia jamii kutoka Kenya ambazo ziliweza kupoteza wapendwa wao katika zogo hilo.
Wakiongea siku ya Jumanne katika mji wa Nairobi, mwenyekiti wa Supkem Profesa Abdulghafur El-Busaidy alisema kuwa bado jamii zilizoathiriwa zina machungu ya kuwapoteza jamaa zao.
Alisema serikali yoyote ulimwenguni kunapotokea suala lolote la maafa sharti iwajibikie mikasa na kujitokeza kuwapa waathiriwa fidia.
“Wengi wa jamii iliyoathiriwa ni kutoka mjini Mombasa na sisi kama wapigania haki za waislamu katika nchi ya Kenya hatutanyamaza kutokana na maafa hayo ambayo hadi sasa yameshtua wengi katika nchi husika ambazo zilipoteza jamaa,” alisema El-Busaidy.
El-Busaidy aliitaka serikali ya Saudi kuweka mipangilio ya kusimamia shughuli hiyo ya waislamu ulimwenguni ambayo inafanyika kila mwaka kusherehekea Hajj, ambayo ni siku muhimu katika kalenda ya waislimu.
Aidha, alisema kuwa kumekuwa na ongezeko la idadi ya mahujaji kila mwaka ambao huenda Mekka kwa ajili ya kuhiji, na hivyo kutaka kuwepo kwa mikakati ya kuona kuwa maafa kama hayo yaliyoshuhudiwa mwaka huu, hayatafanyika tena kwa kuwa ni haki ya kila mahujaji kurudi salama kwenye familia yake baada ya Hajj.