Share news tips with us here at Hivisasa

Tawi la Chuo Kikuu cha Moi jijini Mombasa litazindua masomo ya shahada za Uzamifu na Uzamili kwenye hafla itakayofanyika Jumatatu tarehe 12 mwezi huu huku ikilenga kutoa masomo kwa wananchi kote nchini.

Katika taarifa iliyochapishwa kwenye tovuti yao siku ya Alhamisi, chuo hicho kimetangaza kuzindua masomo hayo kwenye Shule za Ujenzi wa Raslimali Watu na Shule ya Biashara na Uchumi.

"Chuo cha Moi kitazindua rasmi masomo ya shahada za Uzamifu na Uzamili katika tawi lake la Mombasa tarehe 12 Octoba mwezi huu," taarifa hiyo ilisoma.

Kulingana na taarifa hiyo, tayari wanafunzi wameanza kujisajili kusomea masomo hayo, huku wengine zaidi wakitarajiwa kujiunga nao.

Hafla hiyo itasimamiwa na Naibu Chansela wa Chuo hicho Prof Richard Mibey akiambatana na Wadiri wa Shule hizo mbili. 

Tawi hilo lilifunguliwa mwaka 2009, wakati huo ikianza na wanafunzi 65, waliosalijiwa kwenye shule hizo kusomea masomo ya Shahada.

"Chuo Kikuu cha Moi ni cha kipekee na kinatoa masomo ya kisasa huku ikilenga kuwapa wanafunzi ujuzi wanayohitaji kunawiri katika soko ya kimataifa," taarifa hiyo ilimalizia.