Mkuu wa Idara ya Ardhi, Makao na Mipangiliyo ya mji katika Kaunti ya Mombasa Francis Thoya, amesema kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati ya kukabiliana na El Nino.
Akizungumza siku ya Jumatano akikagua urekebishaji wa mabomba ya maji taka na mitaro katika eneo la Bamburi mjini Mombasa, Thoya alisema kwamba serikali ya Kaunti ya Mombasa tayari imeanza shughuli ya kurekebisha mabomba ya kupitisha maji taka pamoja na kuchimba mitaro ya kupitisha maji ya mafuriko yanayotokana na mvua ili kuona kwamba wakazi wa kaunti hiyo hawatatizwa na mvua hiyo ya El Nino.
“Tayari tumeanza shughuli ya kurekebisha mabomba ya maji taka na mitaro katika maeneo mbalimbli ya kaunti kuhakikisha wakazi wanaishi katika hali nzuri ili wasiweze kupitia changamoto za mvua ya El Nino inayaotarajiwa kunyesha,” alisema Thoya.
Aidha, alisema kwamba viongozi wa Kamati ya kukabiliana na majanga katika kaunti ya Mombasa wamejiandaa vyema kukabiliana na majanga pindi yanapotokea.
Aliwashinikiza wafanyibiashara pamoja na wakazi kutupa taka katika maeneo yaliyotengwa ili kuzuia uchafuzi wa mazingira.
“Kama serikali ya kaunti ya Mombasa tumejiandaa vyema kukabiliana na majanga pindi yanapotokea kwani tumebuni vitengo maalum tutakavyosaidiana navyo ili kuona kwamba wakazi wa Kaunti ya Mombasa wako salama,” aliongeza Thoya.
Kamati hiyo imewatahadharisha wakazi wanaoishi katika maeneo ya mabonde kuyahama ili kuepukana na mafuriko na maporormoko yanayokisiwa kushuhudiwa iwapo mvua ya El Nino itanyesha.
Thoya alisema kwamba ni jukumu la kila mkaazi kuzingatia tahadhari hiyo ili kuzuia majanga ambayo ni hatari kubwa kwa maisha ya wakazi.
Haya yamejiri huku dalili za mvua ya El Nino zikianza kuonekana licha ya baadhi ya wakazi kupuzilia mbali kushuhudiwa kwa mvua hiyo.
Kulingana na idara ya utabiri wa hali anga, eneo la pwani linatarajia kushughudia viwango ya mvua vya mililita 250.