Share news tips with us here at Hivisasa

OCPD wa Nakuru Kaskazini, Duncan Nguthu, ametoa onyo kwa madereva wenye mazoea ya kuwaachia matatu za usafiri wa umma (PSV) madereva ambao hawana leseni maarufu kama madereva wa 'Squad'.

Akiongea Jumapili kwa njia ya simu, Nguthu alisema oparesheni kali itafanyika na kuwatia mbaroni  madereva wasiozingatia sheria barabarani, baada ya visa kadhaa vya ajali za magari na pikipiki kushuhudiwa kwenye barabara kuu ya Nakuru-Subukia-Nyahururu.

Katika kisa cha asubuhi siku ya Jumapili, kijana mmoja anayesemekana kuwa hana leseni ya PSV alikuwa dereva wa matatu iliyokuwa ikielekea kituo cha kibiashara cha Maili Sita kutoka Heshima ambayo ilihusika katika ajali.

“Usikubali kama mwananchi kuingia katika gari ambalo dereva hana mavazi ya kazi, kwa sababu hiyo ni ishara kwamba sio yeye amepewa jukumu la kuwa na hilo gari barabarani,” Nguthu alisema. 

Gari hilo lilikuwa na watu wawili pekee yake na hakuna aliyeumia wala kutiwa mbaroni kwani wote walitoroka baada ya ajali.

Wakati huo huo, baadhi ya madereva kutoka Sacco la BAHAMA na 3NsTravellers, wamemtaka mwanakandarasi anayeikarabati barabara hiyo kuharakisha kazi yake.

Walisema miaka miwili inaelekea kukamilika baada ya kampuni ya Nyoro Construction Company Limited kupewa kandarasi hiyo ambapo wanadai ni Kilomita 15 peke yake zimekarabatiwa katika muda huo.

“Mwaka wa 2013 walikuwa bado kwa barabara hii, na sasa ndio wamefika Maili Saba. Kando na hayo barabara yenyewe imejaa mabonde na milima kwenye lami, gari inayumba barabarani kila pahali,” dereva mmoja aliyeomba asitajwe alisema.