Siku sita baada ya mkanyagano wa watu katika nchi ya Saudia ambao ulisababisha maafa ya watu zaidi ya watu mia saba, bado wakenya wanane hawajulikani walipo.
Ubalozi wa Kenya nchini humo umeahidi kuwa unaendelea na juhudi za kuwatafuta waliopotea.
Baadhi ya jamii ya waislamu katika mji wa Mombasa wana hofu ya kupotea kwa mahujaji hao na kuomba uchunguzi kufanywa haraka ili kubaini waliko wanane hao.
Fatma Ramah ambaye ni mkaazi wa Kizingo mjini Mombasa, akiwaongoza baadhi ya kinamama wa kiislamu ameitaka serikali kuwajibika na kutoa ripoti kuhusu jinsi uchunguzi unaendelea kuhusiana na kupotea kwa watu hao.
"Serikali sharti ifanye haraka ili kutoa ripoti waliko jamaa hao kwa kuwa bado jamii zao zinasononeka kwa kutowaona jamaa zao tangu mkasa huo kutokea," alisema Ramah.
Ripoti zilizotumwa kwenye vyombo vya habari siku ya Jumanne kutoka kwenye ubalozi wa Kenya nchini Saudi Arabia zilidokeza kuwa wakenya hao hawajulikani waliko huku miili ya wale ambao waliaga dunia ikizikwa siku moja baada ya kifo kulingana na sheria za Kiislam.
Balozi wa Saudia Bwana Mohammed Abdi Mohamud alisema kuwa bado wataendelea na juhudi za kuwatafuta waliopotea na kuwahakikishia waathiriwa kuwa ubalozi wa Kenya nchini humo unaendelea kufanya juhudi ili kupata wakenya hao.
Aliwataka wakenya kwa jumla kuendelea na maombi na kuwatakia faraja wakenya wote ambao walipatikana na maafa hayo na kuitaka serikali ya Saudia kushirikiana na ubalozi huo ili kutafuta watu hao wanane ili kutuliza roho za jamaa ambao wameathirika.