Vijana na kina mama katika eneo bunge la Kitutu Chache kaskazini kaunti ya Kisii wameshauriwa kutumia pesa za hazina ya maendeleo ya vijana na ile ya Uwezo vizuri ili kujiimarisha kimaisha.
Akizungumza siku ya Jumanne wilayani Marani, kiongozi wa hazina ya Uwezo Cyrus Bosire aliwashauri vijana kushiriki vikamilifu katika ujenzi wa taifa na kuinua uchumi kupitia kubuni miradi mbalimbali ya maendeleo, na kujinufaisha kupitia hazina hizo za serikali ambazo zilianzishwa kuwasaidia vijana na kina mama haswa kibiashara.
Kulingana naye, hazina hizo zitakuwa zikisaidia wakenya kupunguza hali ya umaskini, ambao unashuhudiwa nchini.
Pia aliomba wale ambao hawajajiuhusisha na vikundi waweze kujihusisha kwa ili kupokezwa pesa kujiendeleza.
“Rais Kenyatta na serikali za kaunti wamejitolea kustawisha maendeleo kikamilifu nchini kupitia makundi ya vijana na kina mama ili kuafikia maendeleo dhabiti ili kutimiza ruwaza ya mwaka wa 2030,” alihoji Bosire.
Kiongozi huyo alisema nchi ya Kenya haingekuwa na maendeleo kama serikali haingeanzisha hazina ya kukabidhi vijana pesa ili kufanyia biashara.
“Naamini kuwa nchi yetu itainuka kiuchumi ikiwa vijana na akina mama wataendelea na biashara wakitumia pesa za mikopo,”aliongeza Bosire