Wabunge kutoka katika eneo la Kaskazini Mashariki wametishia kujiondoa katika muungano wa JAP iwapo hoja ya kumtimua kiongozi wa walio wengi katika Bunge la kitaifa Bw Aden Duale itawasilishwa na kupitishwa bungeni.
Wabunge hao waliokutana na wenzao wa Kaunti ya Nyeri katika hoteli moja jijini Nairobi siku ya Alhamisi walishikilia kuwa Duale ambaye pia ni mbunge wa Garissa mjini siye wa kulaumiwa kwenye mashambulizi ya hivi karibuni katika eneo la Mandera na maeneo mengine ya Kaskazini Mashariki.
Wabunge wa Nyeri walikuwa wametishia kuwasilisha hoja ya kumtimua Duale kufuatia shambulizi la Mandera ambalo liliwaua watu wengi kutoka kaunti yao na walitaka wenzao kuwahakikishia usalama wa watu kutoka kaunti yao ambao wapo katika eneo la Mandera na Kaskazini Mashariki kwa ujumla.
Seneta wa Nyeri Mutahi Kagwe alisema lengo la mkutano huo lilikuwa ni kushughulikia swala la usalama katika eneo la Mandera na walikua wamebuni mbinu za kukabiliana na utovu wa usalama katika eneo hilo.
Mbunge wa eneo la Fafi Barre Shill alisema kuwa tatizo la ugaidi katika eneo la Mandera ni sawa na mashambulizi ya kigaidi yaliyotekelezwa kwenye duka la Westgate na maeneo ya Mpeketoni katika kaunti ya Lamu na hivyo ni sharti lichukuliwe kama shambulizi lolote la kigaidi nchini.
"Mashambulizi la Mandera halina tofauti na mengine yaliyotekelezwa sehemu zingine kama Westgate na Mpeketoni na watu wa Mandera wamekuwa wakitoa majina ya washukiwa wa ugaidi," alisema Shill.
Wabunge wengine waliohudhuria mkutano huo ni Peter Weru wa eneo bunge la Mathira, Mohamed Elmi wa Tarbaj, Priscilla Nyokabi Mwakilishi wa Wanawake Kaunti ya Nyeri na wabunge wengineo kutoka maeneo hayo.