Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa upinzani wamemtaka Rais Uhuru Kenyatta kuheshimu mahakama za Kenya na kuwalipa walimu nyongeza ya mishahara yao.

Viongozi hao wakiongozwa na kinara wa Ford Kenya Moses Wetangula, walimshtumu Rais Kenyatta kwa kuchezea maisha ya watoto wa wakenya na kumtaka alishughulikie suala hilo la walimu kwa dharura.

Akiongea katika eneo la Chomvu mjini Mombasa, kwenye hafla ya kisiasa siku ya Jumamosi, Wetangula alitangaza msimamo wa upinzani kuwa watabaki kidete kuwatetea walimu ili wapate haki yao ya kulipwa mishahara yao kama maafisa wengine wa umma.

Wetangula alidai kuwa serikali ya Jubilee ina nia ya kuwadhulumu walimu na kumtaka rais kukumbuka kuwa mahakama yayo hayo ndiyo yaliyomtangaza kuwa rais mteule baada ya upinzani kuweka kesi kortini kupinga matokeo ya uchaguzi.

“Haki ya walimu lazima iheshimiwe. Rais Uhuru sharti awape walimu hela ili waende shuleni kuwafundisha watoto ambao wanaendelea kuteseka nyumbani na wengi ambao ni wa wazazi maskini,” alisema Wetangula.

Kwa upande wake, seneta wa kaunti ya Mombasa Omar Hassan, aliwapa changamoto viongozi wa Jubilee kwa kuwaambia kuwa iwapo hawatalipa walimu, wangoje kivumbi kutoka kwa upande wa upinzani.

Aliwataka baadhi ya viongozi ambao alisema wanampotosha rais kuacha kufanya hivyo na kumpa Rais Kenyatta nafasi alete utatuzi kwenye suala hilo kwa njia ya mafikiano.