Share news tips with us here at Hivisasa

Huku vita dhidi ya dawa za kulevya vikiendelea, vijana ambao wanataka kujikwamua kutoka kwenye mnaso huo wametakiwa kujitokeza na kujisalimisha kwenye mamlaka ya polisi au ya mashirika ya kupigana na dawa hizo ili waweze kupata msaada wa serikali.

Akizungumza siku ya Ijumaa, baada ya kuwapokea zaidi ya waathiriwa 40 ambao walijisalimisha katika afisi zao, Julius Kaveta, ambaye ni naibu kamishna wa Mombasa, aliwataka vijana wengine kufanya hivyo kwa hiari yao.

Alisema kuwa kujitoa kwenye matumizi ya mihadarati itawapa vijana hao mwamko mpya na ari ya kutaka kuanza maisha mapya na kujiendeleza kiuchumi.

“Jamii yetu ikija pamoja kwa kushirikiana na mashirika mbali mbali ambayo yanapigana na mihadarati, vita dhidi ya dawa za kulevya vitafanikiwa na watu wataishi kwa mwelekeo wa kijamii na kwa njia za kidini,” alisema Kaveta.

Kaveta aliwarai viongozi na jamii kutoka maeneo athiriwa, kuendelea kusaidiana na mashirika ya kungoa uovu huo kwa kutoa ripoti za kunaswa kwa watu ambao wanajihusisha kwenye usambazaji wa dawa za kulevya mjini Mombasa.

Vile vile baadhi ya wakazi kutoka mitaa mbali mbali waliipongeza serikali kuu na ile ya kaunti kwa juhudi zao dhidi ya kuangamiza janga hilo.

Hatahivyo, hawakusahau kuyapa mashirika ya jamii mkono wa pongezi kwa kuwa nyuma ya serikali kwenye vita hivyo.