Share news tips with us here at Hivisasa

Huenda kampeni dhidi ya dawa za kulevya katika eneo la Pwani iliyozinduliwa na Rais Uhuru Kenyatta ikakosa kufanikiwa baada ya asilimia kubwa ya waathiriwa wa mihadarati kutoroka katika vituo vya matibabu.

Waathiriwa hao zaidi ya 100 walisema walitoroka katika vituo hivyo kutokana na kile walichokitaja kama huduma duni katika vituo walivyopelekwa kujinasua licha ya wao kuwasilisha lalama zao kwa wahusika na kukosa kusaidiwa.

Wakizungumza katika eneo la Kisauni Mjini Mombasa siku ya Jumatatu, waathiriwa hao walisema kwamba wamekuwa wakipewa matibabu ya sindano kila uchao bila ya kupewa chakula ndipo wakachukua hatua ya kutoroka na kurejea mitaani.

“Kitu kikubwa chao ni kutupa sindano ya usingizi, ulale ukiamka una njaa hakuna kula unadungwa sindano nyingine. Kwani sisi itakuwa twadungwa sindano tu hatupewi matibabu na walituambia tukienda kwa vituo vya kurekebishia waraibu wa mihadarati tutashughulikiwa vizuri,” alisema mmoja wa waathiriwa hao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Shirika la kupambana na utumizi wa mihadarati na vileo nchini Nacada, Sheikh Juma Ngao, amewalaumu viongozi wa kisiasa kwa kukwepa jukumu walilokubalia na Raisi Uhuru Kenyatta alipozindua kampeni hiyo eneo la Pwani na kusema kwamba viongozi hao sio waadilifu.

“Viongozi wa kisiasa wameshindwa kuwajibikia jukumu lao walilokubaliana na Raisi Uhuru Kenyatta alipozindua kampeni ya kuwasaka walanguzi na watumizi wa mihadarati. Hatua hiyo ndio imechangia vijana hao kutoroka kwa sababu hao viongozi ndio wangekuwa mstari wa mbele kuwapeleka kwa vituo na kuwashgulikia mpaka warejea katika hali yao ya kawaida,” alisema Sheikh Ngao.

Hata hivyo utafiti umbaini kwamba zaidi ya vijana elfu 25 katika mji wa Mombasa wameathirika na utumizi wa dawa za kelevya hatua ambayo ilichangia kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ili kuwanasua vijana hao na kupata matibabu maalum.