Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wakazi haswa vijana wanaoendesha bodaboda, kutoka Wadi ya Magenche, eneo Bunge la Bomachoge Chache watafaidi kutokana na mradi wa kifedha kutoka kwa Mwakilishi wao David Ogugu.

Mwakilishi Ogugu alisema haya siku ya Jumatano katika ziara ya kukagua miradi inayofadhiliwa na pesa za wadi na ile ya kaunti ambapo aliwataka vijana hao kujiweka katika makundi ili iwe rahisi kupata hela hizo kwanzia msimu wa bajeti ya mwaka 2015 na 2016.

Alisema atatenga hela mahususi kutoka kwa mgao wa basari ili kuwafadhili baadhi ya vijana ambao hawajaenda kupata masomo ya udereva ambapo watajifunza na kupata leseni ya kufuzu kutoka taasisi inayotambulika.

Mwakilishi Ogugu pia aliwahakikishia wakazi wa wadi yake kuwa atatekeleza miradi yote hasa ile ya barabara za eneo lake ambazo tayari alisema zinaendelea kukarabatiwa na kufungua baadhi ya viunga vya barabara kuu kurahisisha uchukuzi wa bidhaa na mazao ya wakulima wa sehemu hiyo kuenda kwenye masoko mbali mbali.

“Nitahakikisha kuwa barabara zetu ni bora na zinapitika kwa urahisi ili mkulima, mpita njia pamoja na wahudumu wa matatu na wale wa bodaboda wafanye biashara ya kusafirisha watu kwa wepesi,” alisema Ogugu.

Mwakilishi huyo vile vile aliweza kuwakabidhi waendeshaji bodaboda hao vikingi na paa za mabati ambayo watatumia kujenga vibanda vya kujikinga dhidi ya jua na mvua katika vituo vya abiria wakati wakisubiria wasafiri.