Waendeshaji bodaboda kutoka eneo la Likoni wamelalamika kuwa wananyanyaswa na maafisa wa polisi ambao hupiga doria katika eneo la Shelly Beach nyakati za usiku.
Waendeshaji bodaboda hao walikasirishwa na kisa ambacho mmoja wa afisa wa polisi anadaiwa kumpokonya kijana wa pikipiki mtambo wake kwa kudai kuwa alikuwa amevunja sheria za trafiki, kinyume na madai ya mwaathiriwa ambaye anasema kuwa aliitishwa hongo na maafisa hao.
Akizungumza siku ya Jumatano, mwenyekiti wa wahudumu wa bodaboda katika steji kuu ya Shelly Beach kuelekea Likoni na maeneo mengine, Hassan Mwamdoe, alisema kuwa maafisa hao huwa wanataka kupewa pesa na vijana wa kuendesha bodaboda kila mara na wakidinda kuwapa, huanza kuwahangaisha kwa madai kuwa wamekosa kutilia maanani utaratibu na sheria zinazofutwa barabarani.
“Baadhi ya maafisa hao hata hutuomba hadi shilingi elfu mbili inapofika saa tatu usiku, ikizingatiwa kuwa kuna baadhi ya vijana hujitafutia hela yao kupitia biashara ya pikipiki nyakati za usiku,” alisema Mwamdoe.
Mwamdoe alitoa wito katika idara ya polisi na serikali ya kaunti ya Mombasa, kujadili suala hilo la kudhulumiwa kwa vijana hao.
Alisema kuwa suala la usama linastahili liangaliliwe kwa umakini na maafisa hao badala ya kuwanyanyasa.