Wahudumu wa bodaboda katika eneo la Zambezi, Kaunti ya Kiambu, wamelalamikia kunyanyaswa kila mara na maafisa wa trafiki.
Wahudumu hao walidai kuwa wananyanyaswa licha ya kuzingatia sheria za barabarani.
Hii ni baada ya mmoja wao kutiwa mbaroni na maafisa wa trafiki katika barabara ya Southern bypass.
Wahudumu wenzake walidai kuwa mwenzao hakuwa na hatia bali maafisa hao walitaka kupewa mlungula.
Akizungumza katika kituo cha bodaboda, mwenyekiti wa wahudumu hao, Bwana David Kung'u, alidai kwamba maafisa wa trafiki wamekuwa na mazoea ya kukula mlungula kutoka kwa waendeshaji bodaboda.
Alidai kwamba tabia hii hasusan hufanyika masaa ya usiku ambapo maafisa hao huwasimamisha wahudumu pindi wanapopitia barabara hiyo.
"Kama nchi twapigana dhidi ya ufisadi lakini hapa chini bado ufisadi unaendelea. Sisi kama waendeshaji bodaboda hatutapeana hongo na tunaomba pia tusinyanyaswe kama hatuna hatia," alisema Kung'u.
Simon Mbithi, mhudumu wa bodaboda, alisema kwamba biashara hiyo imekuwa ni kana kwamba wanakula pamoja na polisi kwa kuwa nusu ya faida ya siku huishia kwa maafisa wa trafiki.
"Sitakana kwamba kwa muda mrefu nimeshiriki ufisadi kwa kuwahonga maafisa lakini sasa imefika mahali ambapo lazima sisi wenyewe tukome kutoa hongo ili pia nao waache hulka hiyo," alisema Mbithi.
Hata hivyo, Komanda wa trafiki katika eneo la Kikuyu Inspekta Elizabeth Wakuloba alikana madai ya ufisadi katika idara yake akisema kwamba hilo ni kilio cha kutafuta kuharibia maafisa jina.
Alisema kwamba wahudumu wa bodaboda wamekuwa wakikiuka sheria sana hasusan usiku wanapojua maafisa hawapo.
Wakuoba alieleza kwamba wahudumu mara nyingi huwa hawana leseni ya kuendesha bodaboda na pia hupatikana wakibeba abiria zaidi ya idadi inayokubalika na sheria.
Inspekta Wakuloba alihakikishia waendeshaji bodaboda kwamba maafisa wake hawatashirki katika ufisadi bali watatekeleza jukumu lao la kulinda usalama barabarani.