Wafanyibiashara katika Kaunti ya Nyamira wameonywa dhidi ya pesa bandia kutoka kwa walaghai wanaodai kuwa wateja wao.
Kamanda wa polisi katika Kaunti ya Nyamira Rhoda Kinanu, alisema kuwa wamepokea malalamishi mengi kutoka kwa baadhi ya wafanyibiashara wanaopewa pesa bandia na watu wanaofika kununua bidhaa kwa duka zao.
Akizungumza siku ya Alhamisi, Kinanu aliwahimiza wafanyibiashara kuwa waangalifu wakati wa kupokea pesa kutoka kwa wateja wao.
"Tumekuwa tukipokea malalamishi kutoka kwa wafanyibiashara mbalimbali kuhusiana nakupokezwa pesa bandia kutoka kwa wanunuzi wa bidhaa. Ninawasihi wafanyibiashara hao kuwa waangalifu wanapo pokezwa pesa hizo,” alisema Kinanu.
Afisa huyo wa polisi aidha amewaonya watu watakao patikana wakisambaza pesa bandia katika Kaunti ya Nyamira akisema kuwa watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
"Nawaonya watu wenye tabia ya kusambaza pesa bandia katika maeneo mbalimbali kuwa yeyote atakaye patikana atachukuliwa hatua kali za kisheria,” alisema Kinanu.
Wito huo umetolewa wiki chache tu baada ya mshukiwa mmoja kukamatwa na maafisa wa polisi katika sehemu ya Kebirigo na noti bandia za takriban Sh100,000.