Watu zaidi ya 1,000 waliofurushwa kwenye majumba waliyokuwa wakiishi wamelalamikia hatua hiyo na kuitaja kama isiyokuwa ya haki.
Watu hao waliokuwa wakihudumu kama wafanyikazi wa Kampuni ya Maua ya Twiga Roses iliyoko mjini Naivasha waliachishwa kazi na kufurushwa na maafisa wa polisi kutoka walikokuwa wakiishi siku ya Jumapili katika hali isiyoeleweka.
“Tuliamkia shugli zetu kama kawaida kisha tukapatana na polisi waliojihami waliokuwa wamejiunga na wahuni wengine na kutuamuru tuhame eneo hilo kwa upesi. Sisi hatukuelewa kilicho kuwa kikiendelea kwani hatukuwa tumejulishwa na kampuni kwamba tunafaa kuhama,” alidai Susan Waithera, mmoja wa wafanyi kazi hao.
Wafanyikazi hao pia walilalamikia kufutwa kazi kabla ya kulipwa mshahara yao, tabia ambayo wanakiri kwamba kampuni yao imezoea kwani ilipokuwa ikibadili jina kutoka Kampuni ya Karuturi hadi ya Twiga Roses iliwafuta kazi watu 2,000 na kukosa kuwalipa marupurupu yao.
“Hii sio mara ya kwanza wanafanya kitendo kama hiki, hapo awali walipobadili jina waliwafuta wengine 2,000 na hawakuwalipa chochote, lakini sisi hatubanduki mahala hapa, tutapiga kambi hapa hadi tutakapojua tumefurushwa kwa sababu gani na kulipwa mshahara yetu,” aliongeza Waithera.
Aliongeza kwamba wengi wa waliofurushwa walikuwa wamefanyia kampuni hiyo kazi kwa muda mrefu huku wengi wao wakiwa hawajapata mshahara yao kwa muda.