Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Asasi za kiafya katika soko la Ko-Owaga, Nyakach zimewaonya wahudumu katika vichinjio eneo hilo kuzingatia afya ya wananchi.

Wahudumu hao wameombwa kukoma kuwauzia wakazi nyama ambayo imepimwa na kupatikana na kasoro. 

Akizungumza siku ya Jumatatu alipokuwa akikagua nyama kwenye buchari za eneo hilo, afisa wa kupima nyama kutoka katika wizara ya afya, Peter Arungu alionya kwamba watakaopatikana wakiwauzia raia nyama ambayo imepimwa na kupatikana na kasoro watachukuliwa hatua kali za kisheria kwa kuhatarisha maisha ya wananchi. 

''Nyama ikisha pimwa na kupatikana na ugonjwa au kasoro yoyote ambayo ni hatari kwa maisha ya binadamu, ni sharti kuzikwa kwenye shimo kulingana na sheria ya afya,'' alisema Arunga.

Mmoja wa wakazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake kutajwa alifichua kuwa baadhi ya wanaofanya kazi katika vichinjio kwenye soko hilo huficha nyama iliyoamrishwa na daktari kutupwa baada ya kupatikana na ugonjwa au kasoro nyinginezo, na kisha baadaye kuwauzia wakazi kwa bei nafuu badala ya kuzika nyama hiyo.

''Tuligundua kwamba hata baadhi ya hoteli za hapa hukimbilia kununua nyama hiyo kutokana na bei yake ambayo ni ya chini sana ikilinganish na bei ya kawaida kwenye buchari,'' alisema mkazi huyo. 

Aidha, wenye buchari walitakiwa kuzingatia afya na usafi kwa kufuatilia wahudumu wao wakati wanapochinja na kutayarisha nyama kabla ya kuwauzia wateja.