Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Wanawake wanaohudumu katika baa na vilabu, mjini Mombasa wamelalamikia kusumbuliwa na maafisa wa polisi ambao huwashika na kuwadhulumu kimapenzi hata bila idhini yao.

Wahudumu hao walidai kuwa kuna mazoea miongoni mwa baadhi ya maafisa wa polisi ambao huingia mahali pao pa kufanyia kazi na kuwasingizia kuwa hawana vibali vya kuhudumu na kuwapeleka hadi kituoni au kwenye baadhi ya nyumba za maafisa hao au majengo fulani, ambapo huwafanyia mapenzi kwa lazima hata bila ya kinga.

Wakizungumza na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumanne, baadhi ya wahudumu hao walisema kuwa wanapojaribu kukataa, wanapigwa na polisi hao, na mara nyingi huwasingizia kuwa walikuwa wanazurura usiku au kuwekewa dawa au bunduki ili iwe ni kama ulikuwa unashirikia katika masuala haramu yaliyo kinyume na sheria.

Jane Mwikali, ambaye uhudumu kwenye klabu moja mjini Mombasa, alisema kuwa amewahi kushikwa mara moja na maafisa hao wakamsingizia kuwa alikuwa anashiriki wizi.

Alipoona kuwa wanamwekea mashtaka ambayo hayapo, ilibidi akakubali kulala na mmoja wao lakini bahati nzuri baada ya kupimwa, alipata alikuwa sawa.

Biriah Golale kwa upande wake alisimulia jinsi mmoja wa rafiki zake alijipata kwenye mashambulizi ya kunajisiwa kwa zamu na maafisa watatu ambapo aliweza kuambukizwa maradhi ya kaswende, na baadaye aliweza kuacha kazi hiyo.

Samson Ogolla, ambaye ni mmiliki wa klabu katika mtaa wa majengo, alisema kuwa visa hivyo viko na mmoja wa msichana wake wa kazi alidhulimiwa lakini alichukua hatua ya kisheria na polisi mhusika aliweza kuhamishwa.

Alitoa wito kwa serikali ya kaunti kuangalia sheria ambazo zitawalinda wahudumu wa baa hasa wale wa kike dhidi ya dhuluma ambazo wamekuwa wakipata.