Kamanda wa polisi katika kaunti ya Nyamira, Abraham Ndegwa amewaonya wahudumu wa magari ya kubeba abiria maarufu kama matatu, dhidi ya kushirikiana na maafisa wa polisi wa trafiki kula hongo pindi wanapovunja sheria.
Akiongea siku ya Jumanne katika mji wa Keroka, Ndegwa aliwashauri wahudumu wa matatu kufuata sheria wanaposababisha ajali au kuwajibikia vitendo vyao kwa kuenda katika kituo cha polisi kilichoko karibu kutoa ripoti badala ya kuhonga afisa wa polisi, hali ambayo alisema kuwa imekita mizizi miongoni mwa wahudumu hao.
Aidha, aliwataka mafisa wa polisi kuwa katika mstari wa mbele kwa kupigana na vitendo vya utoaji hongo, na kuhakikisha jina la idara hiyo linaendelea kusafishwa kimadili kwa vile kitengo kama cha trafiki kimekuwa na lawama nyingi kutoka kwa umma kuhusiana na masuala ya maadili.
“Ningependa kuona madereva pamoja na utingo wao wakitusaidia kupigana na tabia ya kutoa na kupokea hongo ambayo ni kinyume na sheria inayosimamia mienendo na maadili ya maafisa wa polisi kwa jumla,” alisema Ndegwa.
Ndegwa pia alisema kuwa madereva wanapaswa kutumia vituo vya magari inavyopaswa na wajiepushe na kusimamisha magari yao popote bila kuzingatia sheria.
Aliwaonya kuwa watakaopatikana wakigeusha magari kiholela bila kuenda hadi ndani ya steji watashikwa na kushtakiwa dhidi ya makosa ya trafiki.