Wakazi Waislamu kutoka Kaunti ya Mombasa wameshtumu matamshi ya Mfalme wa Saudia Salman bin Abdulaziz al-Saud kwa kudai kuwa maafa yaliyotokea katika mji wa Mecca wiki jana baada ya mkanyagano baina ya mahujaji yalisababishwa na walislamu kutoka Afrika.
Wakazi hao walisema kuwa matamshi kama hayo yana lengo mbaya ni ya ubaguzi wa rangi.
Walisema kuwa si halali kamwe kwa nyakati za sasa watu kuanza kubaguana ikizingatiwa kuwa dini ya Kiislamu inaheshimu haki za kila mmoja bila kuzingatia maeneo wala rangi ya watu.
Walimtaka mfalme huyo kutoa msamaha kwenye jumuia ya Kiislamu kote ulimwenguni kwa kuwadharau na kutoa matamshi ambayo yataleta uhusiano mbaya kati ya dini hiyo.
Wakiongea na mwandishi huyu siku ya Jumatano, katika mji wa Likoni baada ya suala ya asubuhi, wakiongozwa na Jamal Mwinyi, ndugu hao wa Kiislamu walisema huenda matamshi hayo yakaifanya jamii ya Waislamu kutoka nchi za Kiafrika kuwa na utengano miongoni mwao na waislamu wengine kutoka maeneo ya Asia.
Mwinyi alishtumu kitendo hicho na kusema ulimwengu ulishatoka nyakati za ukoloni ambapo watu waliangaliana kwa misingi ya rangi na maeneo ambayo wametoka.
Alisema matamshi kama hayo hayahitaji kusikika kamwe kutoka kwa familia ya ufalme kama ya Saudia ambayo inahitajika kuongoza katika kukemea visa vya ubaguzi wa rangi.
“Hatungetarajia kuwa matamshi kama hayo yangetoka kuto katika kinywa cha mtu kama yeye. Sharti viongozi wawajibike na tunaitaka serikali ya Saudia kuomba jamii ya waislamu msamaha,” alisema Mwinyi.