Wakazi wa Keumbu eneo bunge la Nyaribari Chache, Kaunti ya Kisii wamemuomba mbunge wao kukamilisha ujenzi wa maktaba moja alioanzisha katika mji wa Keumbu.
Wakiongea na Mwandishi huyu siku ya Ijumaa katika Wadi ya Keumbu, wakaazi hao walimshtumu Mbunge wa eneo hilo Richard Tong'i kwa kukosa kukamilisha ujenzi wa maktaba hiyo.
Aidha, wakaazi hao walisema kuwa kuna pesa za maeneo bunge ambazo zinastahili kutumika katika miradi kama huo, lakini bado hazijasaidia katika eneo hilo haswa kukamilishwa kwa maktaba hiyo ili iweze kuwasaidia wananchi wa eneo hilo.
Kwa sasa wamemwomba mbunge huyo kukamilisha ujenzi huo ili waweze kuitumia kama njia moja ya kujiendeleza kimasomo.
"Namwomba mbunge wetu kukamilisha ujenzi wa maktaba hii ambayo imesimama kwa muda sasa maanake kuna pesa za CDF ambazo zinazostahili kutumika katika ujenzi huo na za kufanya miradi zingine kama huu,” alihoji Robert Nyakeri mkazi wa Keumbu.
Wakaazi hao walisema kuwa ujenzi huo amboa ni nyumba ya gorofa itakuwa inawasaidia pakubwa kwani hata ofisi za wadi hiyo zitaweka katika jengo hilo.
"Ujenzi wa Nyumba huu ukikamilika tutaweza kuwa na ofisi zingine katika jengo hili kwani kwa sasa hatuna ofisi katika wadi yetu,” alihoji Truphena Nyang’oga, mkaazi mwingine.
Waliongeza kuwa kutokana na muda mwingi ambao jengo hilo limekuwa likinyeshewa, ujenzi wa jengo hilo sasa unastahili kukamilishwa kabla ya uharibifu wake zaidi.