Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa Mochenwa katika Wadi ya Gesima, Kaunti ya Nyamira wamempongeza seneta wa kaunti hiyo Kennedy Okongo kwa kutoa madawa ya malaria katika hospitali ndogo ya Mochenwa.

Wakiongea hii leo Alhamsi katika hospitali ya Mochenwa kwenye eneo Bunge la Kitutu Masaba wakati seneta Okongo alikuwa akitoa madawa ya malaria iliyogharamia zaidi ya Sh400,000 kama njia moja ya kuinua viwango vya afya juu katika eneo hilo, wakaazi hao walimpongeza kwa hatua hiyo.

"Nampongeza seneta wetu kwa kutukumbuka na kuleta dawa hizi za kupambana na ugonjwa unaotusumbua kila mara," alihoji Milka Nyabuto, mkaazi.

Aidha, wamewaomba wasimamizi wa hospitali hiyo kuwajibika na kulinda dawa hizo zisije zikakosa au kuchukuliwa na wauuguzi wengine kwa nia ya kuziuzia wananchi.

"Nawaomba wasimamizi wa hospitali hii kulinda dawa hizi ili ziweze kutusaidia," alihoji Evans Nyabiba, mkazi mwingine.

Kwa upande wake, seneta Okongo aliiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kununua dawa ili kushughulikia wenyeji wa eneo hilo wanapokuwa wagonjwa.

Okongo alisema kuwa hospitali nyingi katika kaunti hiyo hazina dawa ya kupambana na malaria jambo ambalo ameiomba serikali ya Kaunti ya Nyamira kushughulikia kwa haraka.

"Nawaomba viongonzi wote wa kaunti hii kushughulikia sekta ya afya ili kusaidia wananchi wa kawaida wanapokumbwa na maradhi ya maleria," alihoji seneta Okongo.

Seneta huyo alitoa msaada sawia na huo katika hospitali ya Manga alipowapokeza dawa na vifaa vingine vya afya vya takribani Sh1 milioni.