Madaktari kutoka nchi ya Australia kwa ushirikiano na madaktari wa hospitali ya rufaa na mafunzo ya Kisii walitoa matibabu ya bure kwa wakazi wa Wadi ya Bokimonge.
Wakazi hao 500 walitibiwa bila malipo katika zahanati ya Tongeri iliyoko kwa wadi hiyo.
Kati ya magonjwa ambayo wakazi hao walifanikiwa kutibiwa ni fistula, malaria na saratani ya tumbo.
Akizungumza siku ya Jumatano na waandishi wa habari wakati matibabu hayo yalikuwa yakiendelea katika zahanati ya Tongeri, mkewe gavana wa kaunti ya Kisii Elzabeth Ongwae alisema mradi huo wa kutibu watu bila malipo uliandaliwa na serikali ya kaunti ya Kisii ili kuwakoa watu ambao hawawezi kugharamia matibabu yao.
Aidha, mkewe gavana alizindua mradi wa kliniki ya beyond zero katika eneo hilo huku akisema kliniki hiyo itatoa matibabu kwa watu wa vijiji ambao huwa na shinda kufika katika hospitali za mjini ili kuhudumiwa.
“Watu waliokuja hapa wamefanikiwa kuhudumiwa kimatibabu na kuruhusiwa kwenda nyumbani. Mradi huu uliandaliwa na serikali ya Kaunti ya Kisii na umewawezesha wakazi kutibiwa hata pia ugonjwa wa 'fistula' ambao umekuwa ukiwasumbua baadhi ya wakazi,” alisema Bi Ongwae.
Huduma hiyo ya kutibu watu bila malipo itakuwa katika kanisa ya kiadventista ya Kinuria wadi ya Chitago Borabu eneo bunge la Mugirango Kusini kutoka siku ya Alhamisi hadi siku ya Ijumaa huku watu wakiombwa kujitokeza kwa wingi kutibiwa.