Wakazi wa lokesheni ya Jogoo, ilioko katika Kaunti ya Kisii wametakiwa kuachana na ugemaji na unywaji wa pombe.
Chifu wa lokesheni hiyo alisema unywaji pombe umeleta mizozo miongoni mwa wakazi hata baadhi yao kutaka kujiua.
Akizungumza siku ya Jumatano katika mkutano na wakazi, chifu wa eneo hilo Bwana Richard Magaki, aliwaonya wakazi dhidi ya kunywa pombe haramu na kusema kuwa bado shughuli ya kuwasaka wagema na wanywaji pombe haramu ipo.
“Nawaomba kuepukana na ulevi na kutafuta njia mbadala ya kujiendeleza maishani badala ya kila mara kusingizia kuwa pombe ndio inawapa riziki ilhali munaweza jihusisha na shughuli kama za kilimo na biashara ndogo ndogo za kuuza hata mboga ili kujiinua kiuchumi,” alisema Magaki.
Haya yanajiri siku tatu baada ya mwanamume mmoja kutoka kijiji kimoja cha lokesheni hiyo kujaribu kujiua huku ikisemekana kuwa ulevi wa kupindukia ndio ulimfanya kutaka kutoa maisha yake.
Lokesheni hiyo imetajwa kuwa na kiwango kikubwa cha mizozo ya nyumba na unywaji pombe pamoja na matumizi ya dawa za kulevya jambo ambalo chifu huyo alisema kuwa likikosa kuangaliwa kwa dharura huenda lokesheni hiyo ikaangamia katika lindi la ulevi na dawa za kulevya na kukosa watu wa kufanya kazi kutoka katika eneo hilo.