Wakaazi wa eneo la Kikuyu wamehimizwa kuwapeleka wakongwe kwa matibabu ya macho ambayo yatakuwa bila malipo katika uwanja wa shule ya msingi ya Kikuyu Township hii leo, Jumapili, kwanzia saa tatu asubuhi.
Akizungumza wakati wa matayarisho ya matibabu hayo, naibu wa mkurugenzi mkuu wa shirika lisilo la serikali la Eye Opener Kenya (EOK) Brenda Keriko, alisema kwamba shirika hilo linanuia kuwasaidia wakongwe ambao kwa kawaida wanapozeeka wanazidi kupoteza macho yao.
Alisema pia wengine wanakosa fedha za kuenda kupata matibabu, hivyo basi kukubali kuishi na shida hiyo ya macho.
Mkuu huyo aliongezea kwamba shirika hilo linanuia kuwapa tumaini wakongwe kwa kuwapa matibabu ya bure, huku akiongezea kuwa watalaam wa macho watawashuglikia na hata kuwapa miwani watakayo hitaji bure.
Kulingana na Keriko, macho ni sehemu ya mwili ambayo inafaa kushughulikiwa sana, na kutaja kuwa watoto wanafaa kuangaliwa macho baada ya mwaka mmoja ili wanapokua wasiwe na matatizo ambayo yatakuwa hayakuonekana wakiwa wachanga.
"Tunawahimiza wakaazi wa eneo hili wawalete wakongwe wote kwa matibabu kesho ambayo yatakuwa bure. Zoezi hili ni la muhimu na hatutaki tumwache mkongwe yeyote nje," alisema Keriko.
Hata hivyo, alisema watoto pia watapewa fursa ya kutibiwa pindi tu wakongwe watakapomaliziwa.