Wakazi wa kaunti ya Kisii wameonywa dhidi ya kununua nyama kutoka bucha ambazo hazijaidhinishwa na maafisa wa afya.
Wito huo umetolewa ili kuzuia wakazi kuathiriwa kwa kununua nyama isiyo halali kwa afya ya binadamu.
Akizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne mjini Kisii, afisa mkuu wa mifugo katika kaunti ya Kisii Bernard Mwenga, aliwatahadharisha watu dhidi ya kununua nyama ambayo haijakaguliwa na maafisa wa kukagua nyama.
Aidha, mkuu huyo aliomba watu kununua nyama ile ambayo imepigwa mhuri na kutokula ile ambayo haijakaguliwa na maafisa wa afya.
“Naomba wakazi wanununue nyama ambayo imeidhinishwa na maafisa wa afya ili wajiepushe na madhara ya kukula nyama ambayo si nzuri kwa binadamu,” alisema Mwenga.
Wakati huo huo, afisa huyo aliwaonya wakazi wa Kaunti ya kisii kutotumia madaktari wa kutibu mifugo kama ng’ombe na mbuzi ikiwa hawana kibali cha kuonyesha kuwa wameidhinishwa na kamati ya madaktari wa kutibu mifugo.
Haya yanajiri baada ya kugunduliwa kuwa kuna baadhi ya madaktari wa mifugo amabao ni bandia kwani wengi wao hawana leseni inayoonyesha kuwa wao ni madaktari halisi.
“Kuna watu ambao wanajiita madaktari wa mifugo ambao ni bandia. Naomba kila mwananchi wa Kaunti hii ya Kisii kuwa macho daktari wa mifugo anapokuja kwake ili kutibu mifugo,” aliongezea Mwenga.