Mkurugenzi wa huduma za watoto katika Kaunti ya Nakuru Yusuf Abdi ametoa onyo kali kwa wakazi wanaoishi katika mitaa ya mabanda, wanaowatelekeza watoto wao.
Akizungumza na wanahabari wakati wa operesheni ya Okoa Mtoto mjini Nakuru siku ya Jumatatu, Abdi alisema kwamba watoto wengi wanaendelea kuumia kimya kimya mikononi mwa wazazi wao.
“Wakazi na wazazi wengi kutoka kwa familia za mitaa ya mabanda wamekosa kutilia maanani maslahi ya watoto wao, ikiwemo ya kiafya, kielimu pamoja na makao mbadala,” alisema Abdi.
Abdi aidha alitoa wito kwa wakazi wanaoishi katika maeneo hayo kuripoti visa vyovyote vya watoto wanaotelekezwa kwa maafisa wa polisi au kwa watetezi wa haki za watoto waliyo nyanjani, ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya wale wanaokiuka haki za watoto.