Wakazi vitongojini mwa mji wa Ahero iliyoko Kaunti ya Kisumu siku ya Jumatatu waliishukuru serikali ya kaunti hiyo kwa kuzikarabati barabara zilizoharibika kwenye maeneo hayo.
Ikizingatiwa kwamba baadhi ya barabara hizo zinategemewa sana na wakulima wa mchele, wenyeji walisema barabara hizo zilikuwa hazipitiki, hali ambayo iliwasababishia hasara nyingi wakulima hapo awali.
Hata hivyo, kwa sasa wakulima na wafanyibiashara wameipongeza hatua hiyo, wachukuzi wa bodaboda pia waliipongeza hatua hiyo ya kuzikarabati barabara hizo wakisema kwamba kazi yao ilikuwa ikitatizika kutokana na mashimo yaliyokuwa yamechimbika kwenye barabara nyingi maeneo hayo kufuatia mvua nyingi iliyonyesha msimu uliopita.
Ukarabati huo ulianza kutekelezwa baada ya lalama za majuma machache yaliyopita kutoka kwa wakazi. Barabara kadhaa za kutoka vitongojini kuunganisha mji wa Ahero kama vile, maeneo ya Mariwa, Ombeyi, Kolwa na nyinginezo zinazozunguka maeneo ya mashamba ya mchele zinaendelea kukarabatiwa.
Martin Okoth ambaye ni mhudumu wa bodaboda mjini Ahero, aliwahimiza viongo wa kaunti hiyo kushughulikia maswala yanayoathiri maisha ya wananchi wa kawaida mapema kabla ya hali kuwa mbaya zaidi, kwa kuokoa kuporomoka kwa uchumi wakati raia wanaposhindwa kufanya kazi kwa sababu ya changamoto kama hayo.
''Serikali yetu husubiri hadi pale hali inapowalemea wananchi ndipo waanze kushughulikia jambo fulani. Nawaambia kuchukua tahadhari kabla ya hatari,'' alisema Okoth wakati wa mazungumzo Waandishi wa habari.