Wakazi wa eneo bunge la Borabu katika Kaunti ya Nyamira wamewashukuru viongozi na wanasiasa kwa kuheshimu familia ya waliofiwa kwa kutopiga siasa kwenye mazishi.
Wakizungumza na Wandishi wa habari siku ya Jumapili katika eneo la Metamaywa baada ya shughuli ya mazishi kukamilika, baadhi ya wakazi hao walisema hiyo ndio tabia wanahitaji kutoka kwa wanasiasa na viongozi wakiongeza kuwa hiyo inaonyesha heshima na kuwaomba kuendelea vivyo hivyo.
Hii ni baada ya wanasiasa hao kuepuka kuongengea masuala ya siasa kwenye mazishi ya mtoto wa kamishna wa Communication Authority of Kenya (CAK) Ken Nyaundi siku ya Jumapili katika eneo la Metamaywa iliyoko eneo bunge la Borabu, Kaunti ya Nyamira.
“Tunawapongeza wanasiasa kwa kuepuka na siasa katika sherehe hii ya mazishi na tunawaomba kuendelea na tabia hiyo,” alisema Gladys Mokeira, mkazi.
Marehemu Kezia Nyaundi alifariki kupitia ajali ya barabara katika jijini Nairobi na alikuwa mwanafunzi katika Chuo Kikuu cha Nairobi.
Viongonzi na wanasiasa wengi walifika kwa mazishi hiyo lakini hawakupiga siasa yoyote, jambo ambalo liliwafurahisha wakazi hao.
“Mie nimeridhika jinsi viongozi na wanasiasa wameendesha shughuli ya mazishi bila kutamka lolote la kisiasa. Tunawaomba walio na tabia ya kupiga siasa kwenye mazishi waige mfano wa wanasiasa hawa,” alisema Daniel Ombori mkazi.
Miongoni mwa wanasiasa waliohudhuria mazishi hiyo ni aliyekuwa spika wa bunge la kitaifa Kenneth Marende, Waziri wa Mawasiliano Fred Matiangi, Cyrus Jirongo, Mbunge Joel Onyancha, Mbunge Ben Momanyi, David Chirchir, Charles Nyachae na wengineo.