Wakazi wa eneo la Kikuyu wameshauriwa kuzibua mitaro yote katika eneo hilo, ili kuwa tayari kwa mvua ya El Nino ambayo imetabiriwa kwanzia mwezi wa kumi.
Akizungumza afisini mwake siku ya Ijumaa, Naibu wa afisa wa mazingira bwana Stephen Ng'anga alisema mitaro, hususan ile ipo katika vitongoji duni, inafaa kuzibuliwa ili kuhakikisha maji yatapita bila shida yeyote.
Aliongezea kwamba maji machafu ambayo yamekusanyika na takataka za aina nyingi yana hatari ya kuziba mitaro mvua inapoanza, hivyo basi kuhatarisha maisha ya wakazi.
Aidha, aliongezea kuwa wakazi wachukue jukumu mikonono mwao na kuzibua mitaro hiyo kwa usalama wao.
Aliwashauri wakazi wasipuuze ushauri wa maafisa na badala yake kuzingatia kile ambacho wanashauriwa.
“Afisi ya mazingira pia inahusika pakubwa wakati mvua ya El Nino, tunawashauri wakazi wahakikishe mitaro ni safi ili mvua itakapoanza isizibe kisha kuleta maafa,” alisema Ngan’ga.
Alisema kuwa wwiki ijayo afisi hiyo pia itazuru eneo tofauti na kushauri wakaazi wengine kuchimba mitaro pale panapofaa kwa matayarisho ya mvua hiyo," alisema Ng'anga.