Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa mtaa wa Nubia mjini Kisii wameombwa kuzingatia usafi kama njia moja ya kujingika na magonjwa yanayosababishwa na uchafu.

Akiongea siku ya Jumanne katika eneo la Nubia alipowatembelea wakazi hao kukagua wanavyoishi, mhudumu wa afya ya jamii Kepha King’oina aliwahimiza wakazi hao kuzingatia usafi kila wakati. 

“Kuna magonjwa mengi ambayo yanasababishwa na mazingira chafu kwa hivyo ni wajibu wa kila mmoja wetu kuhakikisha kuwa mahali tunaishi ni pasafi kila wakati,” alisema King’oina.

Aidha, King’oina aliwaomba wakazi hao wawe wanasafisha nyumba zao kila wakati ili kuwazuia funza kwani funzu hupenda nyumba chafu.

Hii ni baada ya kupata mzee mmoja wa miaka 38 akiwa ameathiriwa na funza na kumsaidia kwa kumpa dawa ya kukabiliana na funza hao na kuomba jamii yake kuzingatia usafi wa mazingira na wa kibinafsi.

“Funza hawa huletwa na uchafu kwa hivyo namuomba kila mmoja wetu kuwajibika na kuzingatia usafi kila mara. Watu wanastahili kulala katika mazingira safi," aliongezea Kingo’ina.

Mhudumu huyo aliwaomba wakazi hao kutafuta ushauri wa matibabu kutoka kwa daktari wanapokuwa wagonjwa.

Kepha aliongezea ni lazima watu watoe maji wanaohifadhi kwenye mitungi kama njia mojawapo ya kupambana na ugonjwa wa malaria na kuwaomba wawe wanalala ndani ya neti kila wakati.