Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Wakazi katika eneo bunge la Bochari, Kaunti ya Kisii walilazimika kujiwekea matuta katika barabara ya kutoka Kisii kuelekea Suneka kama njia moja ya kupunguza idadi ya ajali na gari kuendeshwa kwa kasi.

Hii ni baada ya mwanamke mmoja wa umri wa makamo kugongwa na gari katika eneo la Gesonso siku ya Jumanne na kupoteza maisha yake papo hapo katika barabara hiyo ya Kisii-Suneka.

Wakizungumza na waandishi wa habari siku ya Jumanne baada ya kujiwekekea matuta hayo katika eneo la Gesonso, wakazi hao wakiongozwa na Zachary Nyambunde walidai kuwa wamekuwa wakiitisha kuwekewa matuta na serikali ya kitaifa lakini hadi sasa hawajawahi shughulikiwa vyovyote, jambo ambalo liliwalazimu kujiwekea matuta hayo wao wenyewe ili kulinda maisha ya wakazi wengine.

Mwili wa marehemu ulisafirishwa hadi chumba cha kuhifadhi maiti cha Kisii level five.

“Tumekuwa tukiomba tuwekewe matuta katika barabara hili maana gari huendeshwa kwa kasi sana lakini hatuoni lolote likifanywa. Serikali inahitaji maisha ya watu wangapi yapotee ili kutukumbuka?”auliza Victor Omenge, mkazi.

Wakazi hao waliiomba serikali kuweka matuta kwa barabara zote ili kulazimisha gari kutoendeshwa kwa kasi.

Waliongezea kuwa hatua kali yapaswa kuchukuliwa kwa madereva wanaoendesha gari kwa kasi ili kupunguza visa vya ajali kushuhudiwa kila mara humu nchini.