Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baadhi ya wakazi wa Kaunti ya Nyamira wamependekeza kubuniwa kwa hazina ya fedha kuwasaidia mayatima na watoto kutoka familia maskini kwa masomo yao.

Wakazi hao waliwaomba viongozi waliomo mamlakani, haswa wa Kaunti ya Nyamira kubuni hazina ya fedha ya watoto maskini na mayatima ili kuinua viwango vya elimu katika Kaunti ya Nyamira.

Wakiongea na Waandishi wa habari siku ya Ijumaa katika Wadi ya Rigomba, eneo bunge la Kitutu Masaba iliyoko Kaunti ya Nyamira, wakazi hao wakiongozwa na Jackson Omwenga walisema hazina kama hiyo ikianzishwa katika kaunti hiyo, wanafunzi maskini na wale mayatima watanufaika kwa kulipiwa karo.

“Ni idadi nyingi ya wanafunzi ambao wanatoka katika familia maskini na mayatima katika Kaunti hii ya Nyamira, ndio maana tunapendekeza serikali ya Nyamira ianzishe hazina kando na hazina zingine ili wanafunzi hao wapate usaidizi wa karo na kuendelea na masomo yao kama watoto wengine,” alidokeza Felix Ogwano, mkaazi wa Nyamira.

Pia wakazi hao wamewaomba viongonzi kufadhili watoto mayatima ili nao waweze kupata elimu kama wanafunzi wengine.

“Tunawaomba viongonzi wetu wasaidie watoto mayatima na maskini hata kama ni kwa kuwanunulia sare za shule,” alisema Josphine Bosire, mkazi.