Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi wa eneo bunge la Bomachoge Borabu, Kaunti ya Kisii wametoa makataa ya siku tisa kufanyiwa maendeleo la sivyo waandamane hadi ofisi za gavana wa kaunti hiyo kulalamikiwa maendeleo kutofanywa katika eneo bunge hilo.

Makataa hayo yametolewa na wakazi wa eneo bunge hilo wakiwemo waendeshaji bodaboda, wafanyibiashara na wahudumu wa matatu ambao wametishia kuandamana kulamikia maendeleo kurudi nyumba katika kaunti hiyo ya Kisii.

Aidha, wakazi hao wamesema baada ya siku tisa kukamilika, hawatakubali kutozwa ushuru.

Miongoni mwa maendeleo ambayo walisema wanahitaji gavana wa kaunti hiyo James Ongwae awafanyie ni kukarabati barabara za eneo bunge hilo, kutengeza na kujenga vyoo katika masoko mbalimbali, kujengwa kwa maktaba ya vitabu, kukarabatiwa kwa masoko na vibanda vya waendeshaji bodaboda.

Wakizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano, wiki iliyopita katika eneo bunge hilo wakiongozwa na mfanyibiashara Peterson Achachi, wakazi hao walisema tangu serikali za ugatuzi kuanzishwa nchini, wao kama wakazi wa eneo bunge la Bomachoge Borabu hawajafanyiwa maendeleo kikamilifu.

“Sisi kama wakazi tulimpigia Gavana Ongwae kura katika uchaguzi uliopita lakini hakuna maendeleo ametufanyia. Leo tumetoa tishio kuwa kuanzia tarehe 30 hatutakubali kutozwa ushuru maana hiyo ushuru ambayo tumekuwa tukitozwa hatujaona ikifanya maendeleo katika eneo bunge hili,” alisema Victor Mose, mhudumu wa matatu.