Chifu wa Lokesheni ya Mochenwa, Wadi ya Gesima, amewataka wakazi wote kuishi kwa amani bila kuzozana juu ya mipaka ya mashamba yao.
Akiongea siku ya Jumatatu ofisini mwake ilioko Gesima, Chifu Magara Makori alisema kuwa mizozano ya ardhi imepitwa na wakati na wakazi wanapaswa kuishi kwa amani ili kuinua viwango vya maendeleo.
“Natumai huu ni wakati wa kufanya maendeleo na si wakati wa fitina kati ya jamii kwa sababu ya kuzozana juu ya mipaka ya ardhi. Nawaomba wakazi muwaheshimu wenzenu ili tuweze kuinua maendeleo ya lokesheni hii,” alisema Chifu Makori.
Makori aliwaonya wale ambao wana tabia ya kuzozana katika lokesheni hiyo na kuwaomba kukoma tabia hiyo huku manaibu na wazee wakijii wakiamrishwa kuwachunguza na kuwaripoti ili wachukuliwe hatua kali ya kisheria.
Kulingana na mzee wa vijiji vya Kiamitengi na Matunwa, Nyakwana Orogo, watu wengi katika vijiji hivyo wamekuwa wakiwasumbua wajane kwa kuwa na mizozo ya aridhi huku akiwaonya kuwa hatua ya kisheria itachukuliwa didhi yao.
Kwa sasa kila mkazi ameombwa kujiwekea nyua ili kubaini shamba lake linaishia wapi kama njia moja ya kuzuia mizozo ya kila mara.